Mnamo tarehe 2, Disemba, 2020, Idara ya Kiswahili iliandaa webina spesheli kusherehekea miaka 50 tangu chuo kikuu cha Nairobi kilipoanzishwa rasmi.  Mada kuu ya webina hio ilikuwa, “Kiswahili Ulimwenguni.”

Webina hio ya kufana, ilihudhuria na watu  wa tajriba mbali  mbali miongoni mwao wanafunzi wa chuo kikuu cha Nairobi, Wahadhiri na wasomi kutoka pande tofauti tofauti ulimwenguni ikiwemo, Poland, Ghana, Uganda, Tanzania, Mariakani na Uchina.  

Akizungumza katika hafla hio, Naibu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Nairobi , Prof. Stephen Kiama alisema kwamba Chuo Kikuu cha Nairobi kinajivunia kwa kuweza kuchangia pakubwa usambazaji wa lugha ya Kiswahili duniani. “Chuo Kikuu cha Nairobi kimeorodheshwa miongoni mwa vyuo vikuu 10 bora barani Afrika mara kwa mara na tuna furaha kwamba mchango wetu kwa jamii na umaa ni wa kiwango kikubwa Zaidi.” Prof Kiama alizidi kusema kwamba Chuo Kikuu Cha Nairobi kitaendelea kuweka mikakati bora ili kufanikisha uchapishaji, utafiti na uvumbuzi wa lugha ya Kiswahili. “Nina furaha kuwajulisha kwamba wahadhiri na maprofesa wa Idara hii ya Kiswahili wametia fora katika ufundishaji, utafiti na uchapishaji. Ni vigogo wanaotajika ulimwenguni kote na baadhi wameweza kushinda tuzo za kitaifa na za kimataifa.

Naibu Makamu wa Chuo Kikuu cha Nairobi anayesimamia maswala ya Elimu Prof. Julius Ogeng’o katika hotuba yake aliwapongeza walimu na wataalamu wa Kiswahili kutoka Chuo Kikuu cha Naiobi kwa kupeperusha  bendera ya Chuo kikuu ulimwenguni kupitia ufundishaji, utafiti na uchapishaji kwa lugha ya Kiswahili. “Kama tunavyofahamu sote, Kiswahili ni lugha rasmi na lugha ya taifa la Kenya. Kwa hivyo,tunajivunia ukweli kwamba lugha hii inazidi  kusambaa ulimwenguni.” Alisema Prof. Ogeng’o.

Kwa upande wake, msemaji mkuu katika hafla hio Prof. Ngugi wa Thiongo ambaye pia ni mwandishi mtajika alisema kwamba ni muhimu kuweko na sera ambayo imnazipa kipao mbele lugha tatu nchini Kenya zikiwemo, lugha ya mama, Kiswahili na Kiiengereza. Akimnukuu Shabaan Robert, Prof. Ngugi wa Thiongo alisema kwamba, “ Titi la mama litamu, hata likiwa la mbwa, Kiswahili naazimu, sifayo iliyofumbwa, Kwa wasiofahamu, niimbe ilivyo kubwa, toka kwa milizamu, funika palipozibwa, titile mama litammu, jingine halishi hamu.”

Ngugi

Prof.Ngugi wa Thiongo akizungumza katika webina ya "Kiswahili Ulimwenguni"

Dkt Beata Wojtowicz kutoka katika  hotuba yake alisema kwamba Kiswahili kinaenziwa sana Nchini Poland na Kwamba lugha  za Afrika haswa Kiswahili ni muhumu sana katika mawasiliano duniani. .

Mwenyekiti wa Idara ya Kiswahili, Prof. Iribe Mwangi naye alisema kwamba kaulimbiu ya webina hio ilikuwa ni “Kiswahili Ulimwenguni” ambapo madhumuni ilikuwa ni kuzungumzia namna ambavyo Chuo Kikuu cha Nairobi kimechangia katika kukisambaza na kukizagaza Kiswahili ulimwenguni. Prof. Iribe alisema kwamba “Ni muhimu kutaja kwamba kati ya masomo yote tunayoyatoa humu chuoni, ni Kiswahili pekee chenye asili yake humu, masomo mengine yote tumeyakopa. Hivyo basi, kama waghaibuni wametufanyia hisani na kutuletea uhandisi, uhasibu, sheria, utabibu, fizikia, 4 falsafa na maarifa mengineyo, mbona sisi tuwahini kile tunachokimiliki?” Mwenyekiti huyo wa idara ya Kiswahili vile vile alitoa mifano kuonyesha namna ambavyo Kiswahili kilienezwa ulimwenguni katika miaka 50 iliyopita. “Katika miaka ya 70, wasomi kama vile Prof. Mohamed Abdulaziz walieneza Kiswahili Ulaya, hasa Ujerumani na Uingereza. Baadaye, wasomi wengine kutoka chuoni humu kama Maprofesa Wamitila, Rayya Timammy na Kineene walifuata nyayo hizo. Prof. Said Ahmed na Prof. Kineene walieneza Kiswahili Ujapani naye Dkt. Hannah Mwaliwa akakiendeleza Afrika Kusini. Dkt Ayub Mukhwana na baadaye Prof Olali walifunza Kiswahili Uchina. Katika miaka ya themanini, Prof. Kineene alifunza Kiswahili Korea Kusini katika Chuo Kikuu cha Hankuk. Baadaye, walimu wengi wamesaidia kukuza kitengo 5 cha Kiswahili chuoni humo wakiwemo Maprofesa Tom Olali na Kithaka wa Mbera na pia Dkt. Michira. Maprofesa Lisanza Muaka na Iribe Mwangi wamesambaza Kiswahili Marekani Kusini na Marekani Kaskazini. Dkt. Prisca Jerono naye aliwahi kukipeleka Kiswahili Marekani ya Kati na Afrika Magharibi. Maprofesa Mohamed Bakari, Iribe na Mbuthia wote wamewahi kukieneza Kiswahili Uarabuni kwa njia moja au nyingine. Mwisho, Maprofesa Mbatiah na Mberia na pia Madaktari Michira, Mungania na Zaja wote wamewahi kufunza Kiswahili Marekani. Hawa ni baadhi tu ya walimu wa Kiswahili ambao wamekitoa Kiswahili Chuoni (nchini) na kukisambaza ulimwenguni.”

Zaidi ya watu 500 waliandikisha rekodi kwa kuhudhuria webina hio ya “Kiswahili ulimwenguni.”

 

 

Share